Adbox

Wednesday, 5 November 2025

WAFANYABIASHARA KARIAKOO WAHIMIZA AMANI, WAKITAKA WANASIASA KUACHA MALUMBANO


Wafanyabiashara wa Soko la Kimataifa la Kariakoo Jijini Dar Es Salaam wameeleza athari kubwa za kiuchumi na Kijamii zilizotokana na ghasia na vurugu za baada ya uchaguzi Mkuu wa Tanzania wa Oktoba 29, 2025, wakimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa maelekezo yake ya kutaka ulinzi na usalama kuimarishwa na shughuli za kijamii na kiuchumi kurejea katika hali yake ya kawaida.

Bw. Eliezer Wilson, Mjumbe wa Taasisi ya Machinga wa Kariakoo (KAWASO) kwa niaba ya wafanyabiashara wadogo wa soko hilo, ametoa kauli hiyo siku moja mara baada ya kuapishwa kwa Rais Samia, ambapo katika hotuba yake ya awali alikemea vitendo hivyo vya uvunjifu wa amani vilivyotokea Oktoba 29- 31, 2025 kwa baadhi ya watu kuvunja, kuharibu na kutekeleza mali za umma na za binafsi katika mikoa ya Dar Es Salaam, Arusha, Mwanza, Mbeya na Mkoani Songwe.

Naye Mfanyabiashara na Kiongozi wa Wafanyabiashara wa soko hilo Bw. Jabir Makunga 
ameeleza athari za ghasia hizo zilizodumu tangu siku ya uchaguzi Mkuu wa Tanzania Oktoba 29, 2025 kuwa ni pamoja na Vifo na tabu zilizotokana na kukosekana kwa huduma za matibabu kwenye Vituo vya afya kwenye Mikoa iliyokumbwa na ghasia hizo, huduma za usafiri kudorora, mfadhaiko, hofu na wasiwasi, ukosefu wa mahitaji muhimu ya kila siku pamoja na mfumuko mkubwa wa bei za bidhaa muhimu.

Akieleza kuhusu athari kubwa za Kijamii na kiuchumi zilizojitokeza kutokana na vurugu, ghasia na maandamano ya Oktoba 29, 2025 Mkoani Dar Es Salaam, Mfanyabiashara Fadhil Mwango amewataka Vijana kujiepusha na kufuata mikumbo isiyofaa na yenye kuhamasisha kuhusu Uvunjifu wa amani nchini badala yake wafuate taratibu rasmi zilizopo katika kuwasilisha kero walizonazo.

No comments:

Adbox