Wananchi wa Mkoa wa Dar Es Salaam wametoa wito wa matumizi sahihi ya Mitandao ya Kijamii na kujiepusha na utoaji wa maoni na uhamasishaji wa uvunjifu wa amani kupitia Mitandao hiyo, wakiiomba serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kuwasamehe Vijana waliojiingiza katika uvunjifu wa amani kwa kufanya vurugu za Oktoba 29, 2025 katika maeneo mbalimbali nchini.
Kwa nyakati tofauti wakizungumza na Chombo hiki cha habari, Wananchi hao akiwemo Mombeki Gervas na Baraka Nyange, wameeleza pia athari za machafuko na ghasia hizo zilizotokea kwenye Mkoa huo, wakisema mbali ya uharibifu wa miundombinu na mali za umma na za binafsi, wenye familia wamekuwa waathirika zaidi wa ghasia hizo zilizodumu kwa zaidi ya siku mbili.
"Sisi tuna majukumu na zaidi familia zetu. Tofauti na mazoea tuliyokuwa nayo tunapomaliza uchaguzi, Uchaguzi wa mwaka huu umekuja na maandamano na tulikuwa hatuna akiba na maisha ya dar tunayajua huwezi kula bila ya kutoka." Amesisitiza kusema Bw. Mombeki.
Kwa upande wake Bw. Nyange amesema "Hii nchi ni ya kwetu, miundombinu iliyoharibika ni ya Watanzania kwahiyo tunapoharibu miundombinu tunayotumia sisi wenyewe maana yake tunajiumiza wenyewe na tunaumiza uchumi wetu wenyewe." Amesisitiza.
Nyange kando ya kuwataka watanzania hususani Vijana kutumia vyema mitandao ya kijamii nchini kwa maslahi ya Tanzania, amesisitiza pia kulinda na kuitunza miundombinu inayojengwa na serikali nchini, akisema miundombinu hiyo imejengwa kwa faida ya watanzania wenyewe katika kurahisisha shughuli zao za kiuchumi na kijamii.

No comments:
Post a Comment