Adbox

Saturday, 15 November 2025

UPIGAJI KURA NI NJIA YA KHERI NA SALAMA YA KUBADILISHA UONGOZI


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amewashukuru na kuwapongeza Watanzania kwa kujitokeza kwa wingi na kushiriki vyema kwenye mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa Tanzania suala ambalo limeonesha wananchi kuthibitisha kuwa ushiriki wa uchaguzi ndiyo njia ya uhakika na salama ya kubadilisha Viongozi wasioridhika nao.

"Njia nyingine zozote hazina kheri wala salama ndani yake." Amesisitiza Dkt. Samia wakati wa hotuba yake ya ufunguzi wa Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo Ijumaa Novemba 14, 2025 Bungeni Mjini Dodoma.

Dkt. Samia ameipongeza pia Tume huru ya Taifa ya uchaguzi kwa kuendesha vyema uchaguzi Mkuu huu, ukiwa wa kwanza tangu kuundwa upya kwa tume hiyo, akisema kwa mara ya kwanza Wakurugenzi wa Halmashauri hawakusimamia uchaguzi na hakuna Mgombea aliyepita bila ya kupingwa kwenye Majimbo na Kata zilizoshiriki uchaguzi.

"Utaratibu pia uliofanyika wa kuongeza vituo vya kupigia kura ulisaidia sana kuondoa msongamano katika Vituo vya kupigia kura na kwa hakika upigaji wa kura ulirahisishwa sana na haikuchukua muda mwingi kwa wananchi suala ambalo limewafanya baadhi ya waangalizi wa uchaguzi kudhani kwamba wananchi hawakujitokeza kupiga kura." Amesema Rais Samia.

Aidha Dkt. Samia pia ameipongeza Tume hiyo kwa namna mchakato wa Kampeni ulivyoratibiwa Vyema, akisema wagombea wote na Vyama vyao vya siasa vilivyoshiriki uchaguzi hakuna aliyekosa uwanja wa kufanyia kampeni.

No comments:

Adbox