Mbunge wa Jimbo la Isimani Mkoani Iringa kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi Mhe. William Lukuvi amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan hajakosea kumteua Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania kutokana na weledi, uwezo wa uzoefu wake katika uongozi nchini.
Lukuvi, Miongoni mwa wanasiasa wa muda mrefu kwenye Bunge la Tanzania ameutaja ubobevu wa kitaaluma wa Dkt. Nchemba kama sababu nyingine muhimu wa yeye kuridhia uteuzi wake, akisema kufanya kwake kazi Benki kuu ya Tanzania kabla ya kuingia kwenye siasa kunathibitisha uwezo mkubwa alionao Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba.
Lukuvi amezungumzia pia uzoefu wa Dkt. Nchemba ndani ya Chama Cha Mapinduzi, akisema amekuwa Mjumbe wa Halmashauri kuu kwa miaka mingi, Mjumbe wa kamati kuu na Mjumbe wa sekretarieti ya Chama hicho pamoja na kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi kati ya mwaka 2012-2015.
Leo Alhamisi Bunge la 13 la Tanzania limemthibitisha Dkt. Mwigulu Nchemba kuwa Waziri Mkuu kwa kura 369 kati ya kura 371 zilizopigwa na sasa kulingana na taarifa ya Ikulu Mteule huyo ataapishwa Ijumaa ya Novemba 14, 2025 Ikulu ya Chamwino Mkoani Dodoma.


No comments:
Post a Comment