Adbox

Wednesday, 19 November 2025

CCM YAAPA KUWACHUKULIA HATUA VIONGOZI WAZEMBE, YAANZA VIPIMO VIPYA VYA UWAJIBIKAJI


Na Sebastian Mavyeo, Dodoma.📍

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema hakitasita kuchukua hatua kali dhidi ya viongozi wazembe, wala rushwa na wale wote watakaoshindwa kuwajibika ipasavyo kwa wananchi, kikisisitiza kuwa nidhamu na utendaji wenye matokeo ndiyo msingi wa uongozi katika serikali na chama.

Akizungumza jijini Dodoma, Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenan Kihongosi, alisema chama kimejipanga kuanzisha vipimo maalum vya kutathmini utendaji wa viongozi katika ngazi zote ili kuhakikisha maelekezo ya Mwenyekiti wa Chama, Rais Samia Suluhu Hassan, yanatekelezwa kwa ufanisi.

Kihongosi alisema Mawaziri na Manaibu Waziri walioteuliwa na Rais wanapaswa kwenda sambamba na kasi ya utendaji wa kiongozi wa nchi, akibainisha kuwa uteuzi wao ni heshima lakini pia una jukumu kubwa la kutekeleza kazi kwa matokeo yanayoonekana kwa wananchi.

“Rais hana mzaha katika masuala ya utumishi wa umma. Viongozi wote lazima wafanye kazi kwa kasi, uadilifu na matokeo. Yeyote atakayekwenda kinyume na maelekezo ya Rais, hatua kali zitachukuliwa,” alisema.

Aidha, Kihongosi alisisitiza kuwa CCM kipo bega kwa bega na Mwenyekiti wake ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuhakikisha amani, utulivu na maendeleo vinaimarika nchini.

Katika hatua nyingine, aliwapongeza viongozi walioapishwa akiwemo Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi, Dk. Emmanuel Nchimbi na Waziri wa Fedha Mwigulu Nchemba, akiwataka kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na kwa kuzingatia masilahi ya wananchi.

Akizungumzia hatua ya Rais Samia kuomba vijana waliokamatwa kutokana na vurugu za Oktoba 29 waachiwe, Kihongosi alisema kitendo hicho kinaonesha uongozi wa busara, huruma na utulivu. 

Pia alisifu uundwaji wa timu maalum ya kuchunguza vurugu hizo pamoja na ahadi ya Rais ya kuanzisha mchakato wa Katiba Mpya ndani ya siku 100.

Kihongosi aliongeza kuwa ndani ya siku 11 tangu mabadiliko kufanyika, tayari ajira zimeanza kutolewa, hospitali zimekatazwa kutoza malipo yasiyo rasmi ikiwemo ada za kuweka maiti, na huduma za umma zimeelekezwa kutolewa kwa haki bila usumbufu kwa wananchi.

No comments:

Adbox