Adbox

Saturday, 15 November 2025

TAIFA LAPATA TUMAINI JIPYA KUPITIA HOTUBA YA RAIS SAMIA


Na Mwandishi wetu, Dodoma

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika lisilo la Kiserikali linalo shughulikia watu wenye ulemavu la Disability of Hope Maiko Salali (FDH)amepongeza hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliyoitoa  bungeni, akisema imekuwa ni mwanga mpya kwa taifa lililopitia mtihani mzito katika kipindi cha uchaguzi.

Ametoa pole kwa Watanzania wote kwa changamoto na maumivu yaliyotokea katika kipindi hicho, akisisitiza kuwa chini ya uongozi wa Rais Samia, taifa litapita salama na kurejea kwenye mshikamano.

Akichambua hotuba ya Rais Samia amesema imejibu matarajio na mahitaji ya Watanzania, hasa yale yanayohusu kuponya majeraha, kurejesha imani, na kufungua ukurasa mpya wa maridhiano ya kitaifa.

Ameeleza kuwa hotuba hiyo ilisubiriwa kwa hamu kubwa na imekuja kujibu maswali yote yaliyokuwa yakizungumzwa na wananchi kwa muda mrefu.

“Rais amefungua mlango wa mazungumzo na hii ina maana kubwa — Tanzania ina kiongozi msikivu, anayejali watu wake na anayetamani kuona nchi inaendelea mbele kwa umoja,” amesema.

Amegusia pia athari zinazowakumba watu wenye ulemavu pindi kunapotokea uvunjifu wa amani amesema,asiyeona hawezi kukimbia hatari,kiziwi anaweza asisikie tahadhari, kwa ujumla, kundi hilo ndilo huwa katika hatari zaidi wakati wa vurugu, "ameeleza

Amesema hatua ya Rais Samia ya kutoa msamaha na kuwaachia huru vijana waliowekwa ndani inaonekana kama tiba ya majeraha , hasa kwa makundi kama watu wenye ulemavu ambao huathirika moja kwa moja wakati amani inapotea.

Kiwanja cha maridhiano, amesema, kinatoa fursa ya taifa kujiponya na kurejesha nguvu ya pamoja. Ameongeza kuwa watu wenye ulemavu wanampongeza Rais kwa uamuzi wake wa busara na kwa kuonyesha uongozi unaotanguliza maelewano kuliko migawanyiko.

Akitoa wito kwa vijana, amekumbusha kuwa walinzi wakuu wa nchi ni vijana wenyewe, hivyo wanapaswa kujilinda kwa kujiepusha na mambo yanayoweza kuivuruga Tanzania au kupandikiza mgawanyiko.

“Tutofautiana kwa mitazamo, ndiyo demokrasia,lakini tusitofautiane mpaka kuliumiza taifa.”amesema

Amewataka viongozi wa kisiasa kuona kipindi hiki si cha kunyoosheana vidole, bali ni muda wa kurejesha utamaduni wetu wa amani, upendo na umoja  misingi ambayo imeijenga Tanzania kwa vizazi vingi.

No comments:

Adbox