Adbox

Friday, 21 November 2025

TIRA YAITAKA JAMII KUONDOA DHANA POTOFU KWAMBA BIMA NI YA MATAJIRI"

MAMLAKA ya Usimamizi wa Bima Tanzania(TIRA)imetoa rai kwa vyombo vya habari nchini kuunga mkono jitihada za TIRA katika kutoa elimu ya bima kwa umma ili kuondoa dhana ya upotoshaji kuhusu ukubwa wa gharama za bima,ucheleweshaji wa malipo pamoja na dhana ya kuwa bima ni kwajili ya matajiri tu kitu ambacho siyo kweli.

Wito huo umetolewa jijini hapa jana na Kamishna wa Bima Dkt.Baghayo Saqware wakati akifungua mafunzo ya Wahariri wa Habari Tanzania kuhusu masuala ya Bima na Umuhimu wa Taarifa ya Soko la Bima.

Dkt.Baghayo alisema Elimu ni ufunguo wa kuongeza uelewa na matumizi ya bima nchini hivyo alitoa wito kwa wahariri 
Kuongeza weledi katika uandishi wa masuala ya bima.

"TIRA ipo tayari kushirikiana nanyi katika kutoa mafunzo na taarifa muhimu,Toeni kipaumbele kwa habari za bima. Haya ni masuala yanayogusa maisha ya wananchi wote kutoka mfanyabiashara mdogo hadi mwekezaji mkubwa.

"Fichueni Wadanganyifu katika bima kwa kufuatilia kwa karibu kesi mbalimbali zinazoendelea kwenye Mahakama zetu. Endeleeni kutumia Taarifa ya Soko la Bima kama nyenzo ya uchambuzi wa habari na  taarifa hizi ni msingi mkubwa wa uandishi wenye tija,"alisema Dkt.Baghayo.

Aidha alisitiza kuwa ushirikiano kati ya TIRA na vyombo vya habari ni muhimu sana katika kuifanya sekta ya bima kuwa chachu ya maendeleo ya taifa.

Hivyo alisema Kupitia majadiliano kama hayo,wanaweza kujenga taifa lenye uelewa mpana wa bima, kuongeza matumizi ya huduma hizi, na hatimaye kuimarisha ustawi wa wananchi.

Kwa upande wake Msuluhishi wa Migogoro ya Bima Tanzania kutoka Ofisi ya Usuluhishi wa Migogoro Tanzania(TIO),Margaret Mngumi alisema kuwa TIO imekuwa kiungo muhimu kati ya wananchi, kampuni za bima na Serikali, na imechangia kwa kiasi kikubwa katika kuimarisha uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika utatuzi wa migogoro ya bima hapa nchini.

Huku akitaja lengo kuu la uwepo wao katika mafunzo hayo kuwa ni kuweka msingi imara wa ushirikiano kati ya TIO na vyombo vya habari ili kwa pamoja kuijenga Tanzania yenye uelewa mpana zaidi kuhusu haki, wajibu na taratibu za kudai fidia za bima.

"Vyombo vya habari vina nafasi ya kipekee katika,Kufikisha elimu sahihi kwa wananchi kuhusu hatua za kudai fidia,Kusaidia kupunguza malalamiko yasiyo na msingi kwa kutoa taarifa sahihi, Kuelimisha umma dhidi ya udanganyifu wa madai ya bima (insurance fraud) na Kuimarisha uwajibikaji wa kampuni za bima kupitia uandishi wa uwazi na wa haki,

"TIO inatambua nguvu mlizo nazo, na tungependa leo tuanzishe ukurasa mpya wa ushirikiano, ili kuboresha zaidi mazingira ya utatuzi wa migogoro ya bima kwa maslahi ya Watanzania,"alisema Mngumi. 

Pamoja na hayo Mngumi alisema kuwa 
Kwa niaba ya Ofisi ya Msuluhishi wa Migogoro ya Bima,wako tayari kufanya kazi bega kwa bega na waandishi, wahariri na vyombo vya habari vyote katika kusambaza elimu, kutoa taarifa za kitaalamu na kushirikiana katika kutatua changamoto zinazoathiri sekta ya bima.

Mwisho.

No comments:

Adbox