Adbox

Friday, 22 August 2025

TBN Yajumuika na Viongozi wa Habari Kuelekea Uchaguzi 2025

8/22/2025 12:12:00 pm


IMG-20250821-WA0061
Dar es Salaam, Agosti 21, 2025: 

WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Paramagamba Kabudi, ametaja majukumu makuu matano ambayo sekta ya habari nchini inapaswa kuyatekeleza kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, akisisitiza umuhimu wa taaluma, weledi na maadili katika kuripoti.

Akizungumza kwenye Mkutano wa Wadau wa Sekta ya Habari na Utangazaji Kanda ya Mashariki uliofanyika jijini Dar es Salaam, Profesa Kabudi alisema vyombo vya habari ni mhimili muhimu katika kukuza demokrasia na kulinda amani wakati wa uchaguzi.

“Vyombo vya habari vinapaswa kuhakikisha wananchi wanajua haki na wajibu wao, kutoa elimu juu ya sera za wagombea, kufuatilia ukiukwaji wa sheria za uchaguzi, kuhamasisha ushiriki wa makundi maalum kama vijana na wanawake, na kupambana na taarifa potofu badala ya kuzisambaza,” alisema Profesa Kabudi.

IMG-20250821-WA0057
IMG-20250821-WA0059

Aidha, alisisitiza kuwa utekelezaji wa majukumu hayo lazima uongozwe na misingi ya taaluma na maadili ya uandishi wa habari ili kulinda heshima ya tasnia na kuepusha vurugu au uvunjifu wa amani.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari, Wakili Patrick Kipangula, alikumbusha waandishi wa habari kuhakikisha wanakuwa na ithibati kabla ya kufanya kazi za kihabari, hususan katika kuripoti uchaguzi.
IMG-20250821-WA0028
IMG-20250821-WA0031
IMG-20250821-WA0030

“Kifungu cha 19 cha Sheria ya Huduma za Habari kinasema bayana kuwa mtu yoyote anayetaka kufanya kazi ya uandishi ni lazima awe amepewa ithibati na Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari. Hivyo ni kosa la jinai kwa mwandishi wa habari kufanya kazi bila ithibati,” alisema Kipangula.

Aliongeza kuwa uhalali wa waandishi wa habari katika kipindi hiki ni jambo lisiloweza kupuuzia, kwani tasnia hiyo inahusisha majukumu makubwa yanayoathiri utulivu wa taifa.
IMG-20250821-WA0046(1)
Mkutano huo uliwahusisha wadau mbalimbali wa sekta ya habari na utangazaji, ambao walijadili nafasi ya vyombo vya habari katika kulinda maadili ya kitaifa na kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025.
IMG-20250821-WA0058
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Mwaluko Kabudi (wa nne kutoka kushoto waliokaa), akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi na wadau wa sekta ya habari na utangazaji baada ya kufungua Mkutano wa Wadau wa Habari na Utangazaji Kanda ya Mashariki uliofanyika jijini Dar es Salaam. Waliokaa kutoka kulia ni Meneja wa Huduma za Utangazaji wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Mhandisi Andrew Kisaka, Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari Patrick Kipangula, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) Rodney Mbuya, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari Gerson Msigwa, pamoja na Kamishna na Msemaji wa Jeshi la Polisi, DCP David Misime pamoja na Mjumbe wa Kamati ya Amani ya Mkoa wa Dar es Salaam. 

Waliosimama nyuma ni viongozi wa Mtandao wa Wanablogu Tanzania (TBN) akiwemo Muhidin Issa Michuzi (Mdhamini), Mwenyekiti wa TBN Beda Msimbe, Mjumbe Joachim Mushi na Mweka Hazina ambaye pia ni Mtaalamu wa Habari, Cathbert Kajuna.

Thursday, 21 August 2025

MWENYEKITI WA CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM) DKT. SAMIA SULUHU HASSAN AONGOZA KIKAO CHA KAMATI KUU YA HALMASHAURI KUUYA CCM DODOMA

8/21/2025 01:46:00 pm

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiongoza Kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa,kilichoketi leo Agosti 21,2025 Jijini Dodoma kwa ajili ya kufanya uteuzi  wa Wagombea  Ubunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Wabunge wa Viti Maalum,Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Viti Maalum.



Monday, 4 August 2025

WAKAZI 8000 KUNUFAIKA NA MRADI WA MAJI KUTOA ZIWA VICTORIA

8/04/2025 09:10:00 pm
Na Lucas Raphael,Tabora

Mradi wa upanuzi wa majisafi ya Ziwa Victoria toka Makomero hadi Mgongoro utawanufaisha Zaidi ya wakazi 8000 wa vitongoji viwili na kijiji kimoja Wilayani Igunga mkoani Tabora.  
 
Akizungumza kabla ya kuzinduliwa mradi huo uliogharimu Shilingi 840 milioni ambao uliwekewa jiwe la msingi na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa,mkurugenzi mtendaji wa Mamlaka ya majisafi na usafi wa mazingira mjini Igunga,Iguwasa,Alex Ntonge  alisema unawanufaisha wakazi ambao walikuwa wakihangaika kutafuta maji.
 


Alieleza kuwa wakazi wa maeneo hayo wamekuwa wakipata changamoto kubwa ya maji na kuwafanya watumie muda mqingi kuhangaikia maji.
 
Kwa sasa alisema adha waliyokuqa nayo wakazi hao imeisha kwani wanapata huduma ya majisafi na salama kupitia mradi huo.
 


Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru 2025,Ismail Ali Ussi,aliipongeza Iguwasa kwa kuhakikisha wakazi wake wanapata maji na kusema kuwa sekta ya maji inafanya kazi nzuri.
 
Alisema Rais Samia Suluhu Hassan amefanya kazi nzuri ya kuhakikisha fedha nyingi zaidi zinaenda sekta ya maji ambayo nayo haijamuangusha kwa kuwa na miradi yenye ubora.
 
Alieleza kuwa watumishi wa sekta hiyo wanafanyankazi nzuri sana na hawana budi kupongezwa kutokana na utendaji aao mzuri wa kazi.
 
Mkuu wa Wilaya ya Igunga,Sauda Mtondoo alisema kukamilika kwa mradi huo kunafanya wakazi wanaopata majisafi na salama mjini Igunga kufikia asilimia mia moja.
 
Mwisho.
 

TAKUKURU YATOA WITO KWA WATUMISHI NA TAASISI SIMAMIZI ZA MAADILI KUSHIRIKIANA

8/04/2025 08:49:00 pm
Doreen Aloyce Dodoma

Watumishi wa Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa(Takukuru) , taasisi simamizi za maadili pamoja na mamlaka simamizi za maadili ya kitaaluma wametakiwa kuendelea kushirikiana na kuwekeza kwenye mikakati ambayo itaakisi na kuimarisha utendaji kazi wa wataalamu wanaotoa huduma kwa wananchi.

 Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Crispin Chalamila,
wakati alipokuwa akifungua kikao kazi cha siku mbili cha kubadilishana uzoefu kuhusu masuala ya maadili na utawala bora baina ya taasisi simamizi za maadili ya utendaji na mamlaka simazi za maadili ya kitaaluma.


Chalamila amesema kuwa uwepo wa mawasiliano baina yao utasaidia kuimarisha hali ya uadilifu katika maeneo yao na kuchukua hatua kwa wale wachache watakaoonekana kwenda kinyume na utaratibu uliowekwa.

“Ninatoa rai kwetu wote kwamba, mawasilisho na majadiliano yetu yatuongoze kwenye ubunifu wa mikakati ya kuboresha misingi ya maadili ya utendaji na maadili ya kitaaluma kama njia mojawapo ya kuimarisha utoaji wa huduma katika utumishi wa umma, kudhibiti vitendo vya rushwa kwa lengo la kuleta ustawi kwa wananchi,”
alisema Chalamila

Hata hivyo, aliwasihi washiriki wa kikao hicho kuendeleza mawasiliano na ushirikiano kati yao taasisi simamizi za maadili pamoja na mamlaka simamizi za maadili ya kitaaluma ili kuimarisha hali ya uadilifu katika maeneo yao na kuchukua hatua kwa wale wachache watakaoonekana kwenda kinyume na utaratibu uliowekwa.

Mkurugenzi wa Usimamizi wa Maadili Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Felister Shuli, alisema kwa mujibu wa utafiti uliofanya mwaka 2021 na ofisi hiyo ulibaini kuwa suala la maadili nchini linaendelea kuimarika.

“Utafiti ule ulionyesha kuwa suala la maadili nchini linaendelea kuimarika kwani wananchi wengi hivi sasa wanaripoti matukio ya ufunjifu wa maadili lakini pia watumishi wa umma hivi sasa wanazingatia suala la maadili ya utumishi wa umma kazini,”alisema

Alisema licha ya mafanikio hayo bado zipo changamoto chache ikiwamo kwenye ngazi ya familia hivyo ipo haja ya kuendelea kukumbushana ili kuboresha utoaji huduma kwa wananchi.

Baadhi ya taasisi zilizoshiriki kwenye kikao hicho ni pamoja na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU),Ofisi ya Mkaguzi Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG),Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora,Mamlaka ya Udhibiti Manunuzi ya Umma (PPRA), Bodi ya Mkandarasi (CRB),Bodi ya Baraza la Wakunga na Wauguzi (TNMC).

Mwisho

Tuesday, 29 July 2025

WATUMISHI OFISI YA WAZIRI MKUU WATAKIWA KUONGEZA BIDII KATIKA KUTEKELEZA MAJUKUMU YAO.

7/29/2025 12:30:00 pm

NA.MWANDISHI WETU - DODOMA

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi amewaasa Watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu kuendelea kufanya kazi kwa bidii na weledi mkubwa katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.


Ameyasema hayo Tarehe 29 Julai, 2025 wakati akifungua Mkutano na Watumishi wa Ofisi hiyo ambapo alisema kuwa ni  muhimu kuwa na nidhamu ya kazi, kushirikiana na kuendelea kuwa wabunifu katika majukumu ya kila siku, na kuwakumbusha watumishi kuwa kazi wanazofanya zinagusa maisha ya mamilioni ya wananchi, hivyo ni wajibu wa kila mtumishi kuhakikisha anatoa huduma bora na kwa viwango vya juu. 


“Pia, nawasihi kuendelea kujenga mshikamano miongoni mwenu. Tunaposhirikiana, tunajenga nguvu ya pamoja ambayo hakuna changamoto inayoweza kutuzuia. Nawaomba tuendelee kufanya kazi kwa bidii na kwa moyo mmoja. Kumbukeni kuwa, kila mchango wenu una thamani kubwa katika kufanikisha malengo ya Ofisi yetu na Taifa kwa ujumla.” Alifafanua Dkt. Yonazi.


Katibu Mkuu Yonazi aliendelea kusema kuwa, katika kuboresha Ofisi hiyo kwa mwaka wa fedha 2025/2026, Ofisi imeendelea kuboresha mazingira ya kazi kwa kushughulikia changamoto zinazohusu mazingira ya kazi na maslahi ya wafanyakazi ikiwa ni pamoja na  kukuza ubunifu katika utendaji kazi wa kila siku na kuimarisha mifumo bora zaidi ya kufuatilia maendeleo ya kazi na kuhakikisha kila mfanyakazi anawajibika ipasavyo kwa nafasi yake.

Katika Mkutano huo watumishi wataweza kupata Elimu kutoka kwa wataalam wa  Mfuko wa Uwekezaji wa UTT kuhusu umuhimu wa kuwekeza, pamoja na mambo mengine pia watapewa elimu  itakayowakumbusha masuala mbalimbali yanayohusu uzingatiaji wa maadili ya utumishi wa umma, masuala ya Afya hususan homa ya ini na magonjwa yasiyoambukizwa.

Monday, 28 July 2025

CCM INATANGAZA MAJINA YA WAGOMBEA UBUNGE MUDA HUU,MBIVU NA MBICHI KUJULIKANA LEO

7/28/2025 06:09:00 pm
Dodoma

Katibu wa Siasa, mafunzo na uenezi CPA Amos Makala anatarijia kutangaza majina ya wagombea Ubunge, udiwani pamoja na nafasi za uwakilishi wa viti maalum kupitia tiketi ya chama cha mapinduzi kuelekea uchaguzi mkuu wa mwezi Oktoba 2025.

Tembelea DOREEN BLOG NA DOREEN TV mara kwa mara upate habari motomoto na uhakika.



DKT. TULIA AITAKA DUNIA KUKABILIANA NA VIKWAZO VINAVYOWAKWAMISHA WANAWAKE

7/28/2025 05:54:00 pm


Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Mhe. Dkt. Tulia Ackson, ameongoza majadiliano muhimu yaliyoandaliwa na UN Women kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, yaliyolenga kutafuta suluhisho la kudumu kwa changamoto zinazowakabili wanawake na wasichana duniani.



Majadiliano haya yamefanyika  katika Ukumbi wa Mikutano wa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, New York, Marekani. Mjadala umejikita katika kuainisha mikakati bora ya kutekeleza ahadi zilizowekwa katika Ajenda ya 2030, Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), Ajenda ya Wanawake, Amani na Usalama, pamoja na Azimio la Beijing.

Aidha, washiriki wamebainisha kuwa changamoto kama ukosefu wa elimu na mifumo dhaifu ya afya zinaweza kutatuliwa iwapo jamii zitajitahidi kulinda mafanikio yaliyopatikana, kwa kuimarisha mifumo ya kisheria, kisiasa na kifedha kwa ajili ya kuendeleza usawa wa kijinsia.



Katika mchango wake, Mhe. Dkt. Tulia Ackson amesisitiza umuhimu wa kuweka usawa wa kijinsia na utekelezaji wa Ajenda ya 2030 kuwa vipaumbele vya kimataifa, huku akitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuungana katika kukabiliana na vikwazo vinavyokwamisha juhudi za Umoja wa Mataifa katika kuwawezesha wanawake na wasichana. 

Amesisitiza kuwa “wakati wa kuchukua hatua ni sasa”, hasa wakati ambapo dunia inakabiliwa na changamoto nyingi zinazotishia maendeleo ya kijinsia.

Friday, 25 July 2025

RAIS DKT.SAMIA ASHIRIKI MAADHIMISHO YA SIKU YA KUMBUKUMBU YA MASHUJAA DODOMA

7/25/2025 04:13:00 pm
Na Doreen Aloyce, Dodoma


RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Samia Suluhu Hassan ameshiriki maadhimisho ya siku ya kumbukumbu ya mashujaa waliopigania Uhuru wa Tanzania yaliyofanyika Mji wa Serikali Wilayani Chamwino Mkoani Dodoma.

Dk.Samia ameongoza maadhimisho hayo kwakuweka Mkuki na ngao huku  Jenerali Jacob Mkunda akiweka Sime na shada la maua ambapo kiongozi wa Mabalozi ameweka Shada la maua kama ishara yakuwakumbuka mashujaa hao.


Awali kulitanguliwa na mizinga miwili ambayo ilipigwa na kufuatiwa na Wimbo wa Taifa.

Akizungumza kwaniaba ya mashujaa hao,Mwakilishi wa mashujaa waliopigana vita vya kagera Balozi  Brigedia Jenerali Francis Benard Mndolwa amesema anajivunia kuwa mmoja wa wapigania uhuru na kuwa mzalendo Kwa nchi yake na amewasihi wafanyakazi wote kuwa wazalendo.


Nao baadhi ya wananchi wameelezea kuhusiana na siku hiyo ya mashujaa.



Ikumbukwe kuwa siku ya Mashujaa huadhimishwa kila Mwaka mnamo Julai 25 kwa kuwakumbuka Mashujaa wote ambao walitoa maisha yao kwaajili ya kupigania uhuru kwa kulinda amani na heshima ya nchi.


MWISHO

Thursday, 24 July 2025

JAB Yakabidhi Press Card kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Michuzi Media Group

7/24/2025 05:57:00 pm
IMG-20250723-WA0078
IMG-20250723-WA0081
●Waandishi Wengine Watakiwa Kuhakiki Viambatisho Katika Mfumo


Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam


Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB), Wakili Patrick Kipangula, amemkabidhi rasmi Kitambulisho cha Uandishi wa Habari (Press Card) Mkurugenzi Mtendaji wa Michuzi Media Group, Muhidin Issa Michuzi, kwa niaba ya waandishi wengine wanaoendelea kukamilisha taratibu za kupata vitambulisho hivyo.


Hafla ya makabidhiano hayo imefanyika jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa jukumu la Bodi hiyo katika kuhakikisha kuwa waandishi wote nchini wanakuwa na vitambulisho halali kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Habari Na. 12 ya mwaka 2016.


IMG-20250723-WA0072
IMG-20250723-WA0079
Akizungumza baada ya kukabidhi kitambulisho hicho, Wakili Kipangula amempongeza Michuzi pamoja na waandishi wengine waliokwishapatiwa vitambulisho vyao kwa kufuata taratibu na kukidhi vigezo vinavyotakiwa kisheria.


Amesisitiza kuwa mchakato wa utoaji wa vitambulisho bado unaendelea na ametoa wito kwa waandishi ambao maombi yao hayajakamilika kuingia katika mfumo rasmi wa Bodi ili kuhakiki viambatisho walivyowasilisha.
IMG-20250723-WA0077
IMG-20250723-WA0073


“Kuna baadhi ya waombaji ambao viambatisho vyao havifunguki, havisomeki, vimerudiwa au havikidhi matakwa ya kisheria kama vile vyeti visivyotambulika au kukosekana kwa barua za utambulisho kutoka kwa waajiri,” amesema Wakili Kipangula.


Ametoa rai kwa waandishi kuhakikisha wanafuata maelekezo yanayotolewa kupitia mfumo kabla ya kuwasiliana moja kwa moja na Bodi kuhusu hali ya maombi yao.
IMG-20250723-WA0074
IMG-20250723-WA0075
JAB imekuwa ikitekeleza jukumu la kuthibitisha na kusimamia maadili ya taaluma ya uandishi wa habari nchini, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanahabari wanatambulika rasmi na kuwa na vitambulisho halali vinavyotolewa kwa mujibu wa sheria.


Michuzi ameishukuru Bodi kwa mchakato huo na kuwataka waandishi wengine kuhakikisha wanazingatia taratibu ili kuimarisha tasnia ya habari kwa weledi na uwajibikaji.

RAIS SAMIA KUWA MGENI RASMI MAADHIMISHO SIKU YA MASHUJAA KESHO JULAI 25 MWAKA HUU

7/24/2025 04:14:00 pm

Na Doreen Aloyce, Dodoma

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Mashujaa yatakayofanyika 25 Julai, 2025 katika Viwanja vya Mnara wa Mashujaa vilivyopo Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma.

Akizungumza leo Julai 24 ,2025 Jijini Dodoma na waandishi wa habari jijini Dodoma kwa niaba ya Kamati ya Maandalizi ya Maadhimisho hayo, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko (Mb), amesema maadhimisho hayo ni alama muhimu ya kuenzi mchango wa Watanzania waliojitolea kwa ajili ya uhuru, amani na maendeleo ya Taifa.



 “Siku ya Mashujaa ni siku ya kitaifa inayotukumbusha uzalendo wa mashujaa wetu  waliolinda mipaka ya Taifa, waliopambana kwa ajili ya uhuru na waliotoa sadaka kubwa kwa ajili ya amani tunayoifurahia leo,” amesema Dkt. Biteko.

Ameeleza Maandalizi ya maadhimisho hayo yamekamilika, huku akisisitiza kuwa Julai 24, 2025 saa 6:00 usiku, Mwenge wa Kumbukumbu ya Mashujaa utawashwa rasmi na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mheshimiwa Rosemary Senyamule kwa niaba ya Rais, kuashiria kuanza kwa siku ya maombolezo ya mashujaa wa Taifa.



Amesema Maadhimisho ya Julai 25 yataanza saa 3:00 asubuhi kwa gwaride rasmi la heshima linaloongozwa na Vikosi vya Ulinzi na Usalama. Usiku wa siku hiyo, saa 6:00, Mwenge wa Kumbukumbu utazimwa rasmi kuashiria hitimisho la shughuli za maadhimisho kwa mwaka huu.

Mbali na hayo Dkt. Biteko ametoa wito kwa wananchi kushiriki kwa wingi katika tukio hilo muhimu kwa historia ya Taifa, akieleza kuwa kila Mtanzania anao wajibu wa kutambua na kuenzi mchango wa mashujaa kwa vitendo vya uzalendo, mshikamano na kuchapa kazi kwa maendeleo ya nchi.



“Tunapoadhimisha siku hii, tunapaswa kujiuliza: Je, sisi kama kizazi cha sasa tunaendeleza misingi waliyoiacha mashujaa wetu? Ushujaa hauishii vitani pekee, bali uko katika kila tendo jema kwa Taifa letu,” amesisitiza.

Amevitaka vyombo vya habari, wanahabari na watumiaji wa mitandao ya kijamii kushirikiana na Serikali katika kuelimisha umma kuhusu maana, historia na umuhimu wa Siku ya Mashujaa.

“Hii ni siku ya kumkumbuka Mtanzania mwenzetu aliyesimama kwa ajili ya wengine,tuwaambie watoto wetu maana ya ushujaa, thamani ya kujitolea, na umuhimu wa kupenda Taifa lao,” amesema Dkt. Biteko.

Maadhimisho ya Siku ya Mashujaa hufanyika kila mwaka nchini kote kama njia ya kuenzi maisha, mchango na maono ya waliolinda uhuru wa Taifa, na mwaka huu 2025, Serikali imepanga kuyafanya kwa heshima, uzito na mshikamano wa hali ya juu.

=MWISHO=

Tuesday, 22 July 2025

NBC Yakutana na Wateja Wake Wakubwa wa Jijini Arusha, Yajadili Fursa, Ufanisi wa Huduma Zake Kwa wateja.

7/22/2025 01:10:00 am


Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imekutana na wateja wake wakubwa kutoka kampuni, wateja binafsi na taasisi mbali mbali (Corporates) wa jijini Arusha ili kujadili fursa za biashara, kutambulisha huduma mpya za benki hiyo sambamba na kuwaejengea uelewa zaidi wateja hao kuhusu faida na manufaa ya huduma hizo. Benki hiyo pia ilitumia fursa hiyo kujadili na wateja hao namna inavyoweza kuboresha huduma zake kulingana na mahitaji yao.

Katika kufanikisha hilo, jana benki hiyo kupitia timu yake ya Biashara na Uwekezaji (CIB) iliandaa hafla maalum ya chakula cha jioni iliyofanyika jijini humo ikiongozwa na Mkurugenzi wa Wateja Wakubwa wa benki hiyo Bw, Elvis Ndunguru sambamba na maofisa wengine waandamizi wa benki hiyo kutoka makao makuu na matawi yake ya jijini Arusha.

Akizungumza kwenye hafla hiyo Bw Ndunguru alisema tukio hilo ni muendelezo wa jitihada za benki hiyo kuendelea kuwa karibu zaidi na wateja wake kwa nia ya kutambulisha huduma zake mpya ikiwemo huduma ya NBC Connect mahususi kwa kundi hilo la wateja, kupata mrejesho wa huduma hizo kutoka kwa wateja hao sambamba na kutoa fursa kwa wateja kubadilishana fursa za biashara.

“Tukiwa kama muhimili muhimu wa utoaji wa huduma za kifedha nchini, NBC tunatambua umuhimu wa utoaji wa huduma bora kwa wateja na kukuza ushirikiano kati yetu na wateja wetu. Hii inasababishwa na mabadiliko yanayotokana na ubunifu na maendeleo ya kiteknolojia tunayoyafanya kila siku’’

“Hivyo hatua hii ya kukutana na wateja wetu wakubwa inatoa fursa kwetu kuelezea maboresho makubwa tuliyofanya kwenye huduma zetu hivi karibuni sambamba na kutambulisha huduma mpya zilizorahisishwa zaidi kidigitali na zinazoendana na mahitaji ya wateja wetu.’’ Alisema

Aidha, kupitia mpango huo benki hiyo imekuwa ikielezea mikakati yake mipana inayolenga kuwahudumia kwa ufanisi zaidi wateja hao, kuwajengea mitandao ya kibiashara miongoni mwao sambamba na kuwasogezea huduma za kibenki karibu zaidi huku huduma ya NBC Connect ikitajwa kama suluhisho muhimu katika kuwasogezea huduma za kibenki wateja hao wakubwa yakiwemo mashirika na kampuni binafsi, pamoja na taasisi za serikali.

“Tunaamini kuwa msingi wa huduma za kipekee ni kuelewa mahitaji na matakwa ya wateja wetu, matukio kama haya yanatupatia mitazamo au maono yanayotusaidia kuwa wabunifu zaidi na kuboresha uzoefu wa kibenki kwa ujumla.” Aliongeza Bw Ndunguru.

Aidha, Bw Ndunguru alitaja baadhi ya mambo muhimu ambayo benki hiyo imekuwa ikiyazingatia katika kukuza ushirikiano na taasisi za kibiashara hapa nchini kuwa ni pamoja na utoaji wa suluhisho zenye ubunifu katika huduma za kifedha, Ubunifu wa kiteknolojia, Ubia wa kimkakati, Kukuza Ukuaji wa Uchumi pamoja na Uwajibikaji kwa jamii huku kipaumbeke kikiwekwa zaidi kwenye masula ya Elimu, Afya na uhifadhi wa mazingira.

“Hivyo basi NBC tunazialika jumuiya za wafanyabiashara kuangalia fursa na faida za kushirikiana na taasisi hii ya fedha ambayo ina dhamira ya dhati na mafanikio yao, kwa kukuza ushirikiano na kutoa zana zinazohitajika katika ukuaji. NBC inalenga kuwa mshirika mwaminifu anaayetegemewa katika biashara hapa nchini,’’ alibainisha.

Wakizungumzia hatua hiyo baadhi ya wateja wa benki hiyo mkoani Arusha walisema imekuja wakati muafaka hasa katika kipindi hiki ambacho mkoa huo upo kwenye mapinduzi makubwa ya kiuchumi kutokana ustawi mkubwa wa sekta ya utalii ikiwa ni matunda ya jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan kupitia mkakati wake wa Royal Tour.

“Kwa sasa mkoa wa Arusha tupo kwenye kasi kubwa ya mabadiliko ya kiuchumi yanayochagizwa na ukuaji wa sekta ya utalii, biashara, kilimo na viwanda. Ni habari njema kwetu kuona kwamba benki ya NBC ambayo inatuhudumia wadau wengi kwenye sekta hizi inatuunga mkono kupitia huduma zao za kisasa ikiwemo zile za kidigitali ambazo kiukweli zimekuwa msaada mkubwa hususani kwenye huduma za miamala ya kifedha na makusanyo ya serikali,’’ alisema Bw Abdallah Kiwango kutoka Shirika la hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA).


Mkurugenzi wa Wateja Wakubwa wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) Bw, Elvis Ndunguru (kushoto) akizungumza na wageni waalikwa ambao ni wateja wa benki hiyo jijini Arusha wakati wa hafla ya chakula cha jioni iliyoandaliwa na benki hiyo kwa ajili ya wateja wake wakubwa kutoka makampuni, wateja binafsi na taasisi mbali mbali (Corporates) ili kujadili fursa za biashara, kutambulisha huduma mpya sambamba na kuwaejengea uelewa zaidi wateja hao kuhusu faida na manufaa ya huduma hizo. Hafla hiyo iliyoandaliwa kupitia timu ya Biashara na Uwekezaji (CIB) ya benki hiyo ilifanyika jana jioni jijini Arusha.


Mkurugenzi wa Wateja Wakubwa wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) Bw, Elvis Ndunguru (kulia) akibadilishana Mawazo na baadhi ya wateja wa benki hiyo jijini Arusha wakati wa hafla ya chakula cha jioni iliyoandaliwa na benki hiyo kwa ajili ya wateja wake wakubwa kutoka makampuni, wateja binafsi na taasisi mbali mbali (Corporates) ili kujadili fursa za biashara, kutambulisha huduma mpya sambamba na kuwaejengea uelewa zaidi wateja hao kuhusu faida na manufaa ya huduma hizo. Hafla hiyo iliyoandaliwa kupitia timu ya Biashara na Uwekezaji (CIB) ya benki hiyo ilifanyika jana jioni jijini Arusha.





Mkurugenzi wa Wateja Wakubwa wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) Bw, Elvis Ndunguru (katikati aliesimama) akisalimiana na baadhi ya wateja wa benki hiyo jijini Arusha wakati wa hafla ya chakula cha jioni iliyoandaliwa na benki hiyo kwa ajili ya wateja wake wakubwa kutoka makampuni, wateja binafsi na taasisi mbali mbali (Corporates) ili kujadili fursa za biashara, kutambulisha huduma mpya sambamba na kuwaejengea uelewa zaidi wateja hao kuhusu faida na manufaa ya huduma hizo. Hafla hiyo iliyoandaliwa kupitia timu ya Biashara na Uwekezaji (CIB) ya benki hiyo ilifanyika jana jioni jijini Arusha.






Baadhi ya wateja wa benki ya NBC jijini Arusha wakifuatilia hafla hiyo







Mkurugenzi wa Wateja Wakubwa wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) Bw, Elvis Ndunguru (kulia) sambamba na maofisa wengie wa benki hiyo wakizungumza na wageni waalikwa ambao ni wateja wa benki hiyo jijini Arusha wakati wa hafla ya chakula cha jioni iliyoandaliwa na benki hiyo kwa ajili ya wateja wake wakubwa kutoka makampuni, wateja binafsi na taasisi mbali mbali (Corporates) ili kujadili fursa za biashara, kutambulisha huduma mpya sambamba na kuwaejengea uelewa zaidi wateja hao kuhusu faida na manufaa ya huduma hizo. Hafla hiyo iliyoandaliwa kupitia timu ya Biashara na Uwekezaji (CIB) ya benki hiyo ilifanyika jana jioni jijini Arusha.
Adbox