Na Doreen Aloyce, Dodoma
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Mashujaa yatakayofanyika 25 Julai, 2025 katika Viwanja vya Mnara wa Mashujaa vilivyopo Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma.
Akizungumza leo Julai 24 ,2025 Jijini Dodoma na waandishi wa habari jijini Dodoma kwa niaba ya Kamati ya Maandalizi ya Maadhimisho hayo, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko (Mb), amesema maadhimisho hayo ni alama muhimu ya kuenzi mchango wa Watanzania waliojitolea kwa ajili ya uhuru, amani na maendeleo ya Taifa.
“Siku ya Mashujaa ni siku ya kitaifa inayotukumbusha uzalendo wa mashujaa wetu waliolinda mipaka ya Taifa, waliopambana kwa ajili ya uhuru na waliotoa sadaka kubwa kwa ajili ya amani tunayoifurahia leo,” amesema Dkt. Biteko.
Ameeleza Maandalizi ya maadhimisho hayo yamekamilika, huku akisisitiza kuwa Julai 24, 2025 saa 6:00 usiku, Mwenge wa Kumbukumbu ya Mashujaa utawashwa rasmi na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mheshimiwa Rosemary Senyamule kwa niaba ya Rais, kuashiria kuanza kwa siku ya maombolezo ya mashujaa wa Taifa.
Amesema Maadhimisho ya Julai 25 yataanza saa 3:00 asubuhi kwa gwaride rasmi la heshima linaloongozwa na Vikosi vya Ulinzi na Usalama. Usiku wa siku hiyo, saa 6:00, Mwenge wa Kumbukumbu utazimwa rasmi kuashiria hitimisho la shughuli za maadhimisho kwa mwaka huu.
Mbali na hayo Dkt. Biteko ametoa wito kwa wananchi kushiriki kwa wingi katika tukio hilo muhimu kwa historia ya Taifa, akieleza kuwa kila Mtanzania anao wajibu wa kutambua na kuenzi mchango wa mashujaa kwa vitendo vya uzalendo, mshikamano na kuchapa kazi kwa maendeleo ya nchi.
“Tunapoadhimisha siku hii, tunapaswa kujiuliza: Je, sisi kama kizazi cha sasa tunaendeleza misingi waliyoiacha mashujaa wetu? Ushujaa hauishii vitani pekee, bali uko katika kila tendo jema kwa Taifa letu,” amesisitiza.
Amevitaka vyombo vya habari, wanahabari na watumiaji wa mitandao ya kijamii kushirikiana na Serikali katika kuelimisha umma kuhusu maana, historia na umuhimu wa Siku ya Mashujaa.
“Hii ni siku ya kumkumbuka Mtanzania mwenzetu aliyesimama kwa ajili ya wengine,tuwaambie watoto wetu maana ya ushujaa, thamani ya kujitolea, na umuhimu wa kupenda Taifa lao,” amesema Dkt. Biteko.
Maadhimisho ya Siku ya Mashujaa hufanyika kila mwaka nchini kote kama njia ya kuenzi maisha, mchango na maono ya waliolinda uhuru wa Taifa, na mwaka huu 2025, Serikali imepanga kuyafanya kwa heshima, uzito na mshikamano wa hali ya juu.
=MWISHO=




No comments:
Post a Comment