Adbox

Sunday, 1 February 2026

ZARA TOURS YA MOSHI YANG’ARA TENA SERENGETI AWARDS, YAENDELEZA MSURURU WA TUZO ZA KIMATAIFA


Na Jackline Kitogo – ARUSHA

KAMPUNI kinara wa utalii nchini, Zara Tours yenye makao yake makuu mjini Moshi, imeendelea kuthibitisha nafasi yake ya juu katika sekta ya utalii baada ya kunyakua tuzo nyingine muhimu katika hafla ya utoaji wa tuzo za Serengeti Awards, ikiwa ni muendelezo wa mafanikio na mfululizo wa tuzo ambazo kampuni hiyo imekuwa ikizipata karibu kila mwaka.

Tuzo hiyo ni miongoni mwa tuzo 51 zilizotolewa katika hafla kubwa na ya kifahari iliyofanyika usiku wa kuamkia leo katika Hoteli ya Mount Meru, jijini Arusha, hafla iliyowakutanisha wadau wakuu wa utalii kutoka ndani na nje ya Tanzania, wakiwemo viongozi wa serikali, wawekezaji, makampuni ya utalii na washirika wa maendeleo.

Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba, alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo, ambapo aliipongeza sekta ya utalii kwa mchango wake mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa Taifa, uongezaji wa ajira, uvutaji wa fedha za kigeni na kuitangaza Tanzania kimataifa kupitia vivutio vyake vya kipekee.

Akizungumza mara baada ya kupokea tuzo hiyo, Mkurugenzi wa Zara Tours, Bi. Zainabu Ansell, alisema ushindi huo ni matokeo ya kazi kubwa, mshikamano wa timu, ubunifu na ushirikiano imara kati ya sekta binafsi na serikali, hususan katika kulinda na kuendeleza vivutio vya Taifa kama Mlima Kilimanjaro.

“Mafanikio makubwa yanayoonekana katika Mlima Kilimanjaro ni ushahidi wa wazi wa juhudi za serikali kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya utalii. Mazingira ya mlima yameimarika, huduma zimeboreshwa na usalama umeongezeka kwa kiwango kikubwa, hali inayowapa watalii uzoefu wa kipekee na wa kimataifa,” alisema Bi. Zainabu.

Aliongeza kuwa maboresho hayo yameufanya Mlima Kilimanjaro kuendelea kuwa nembo ya utalii wa Tanzania duniani, na kuifanya nchi kuwa miongoni mwa vituo vinavyoongoza kwa utalii wa milima barani Afrika na duniani kwa ujumla.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, ongezeko la idadi ya watalii wanaopanda Mlima Kilimanjaro limechangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa sekta ya utalii, kuimarisha mapato ya Taifa na kuinua maisha ya wananchi wanaonufaika moja kwa moja na shughuli za utalii, huku kampuni kama Zara Tours zikichukua jukumu muhimu katika kuhakikisha wageni wanapata huduma zenye viwango vya kimataifa.

“Ninajivunia sana mafanikio haya. Leo ni siku ya kusherehekea hatua kubwa tulizofikia. Mimi pamoja na timu yangu tumejipanga kikamilifu kuendelea kuinua viwango vya kitaaluma, kuongeza ubunifu, kuwekeza katika rasilimali watu na kuhakikisha Tanzania inaendelea kuvutia watalii wengi zaidi,” alisisitiza.

Bi. Zainabu aliahidi kuwa Zara Tours itaendelea kuwa mshirika wa karibu wa serikali katika kukuza utalii endelevu, kulinda mazingira, kuhifadhi vivutio vya asili na kuitangaza Tanzania katika majukwaa ya kimataifa, sambamba na malengo ya Taifa ya kukuza uchumi kupitia sekta ya utalii.

Kwa ujumla, Serengeti Awards imelenga kutambua, kuthamini na kuenzi mchango wa taasisi, makampuni na watu binafsi waliotoa mchango mkubwa katika maendeleo ya sekta ya utalii nchini, huku ushindi wa Zara Tours ukiongeza heshima na hadhi ya Tanzania katika ramani ya utalii wa dunia.

Mwisho.

No comments:

Adbox