Adbox

Monday, 2 February 2026

PRF. Mbarawa aeleza mafanikio ndani ya siku 100 za Rais Samia Suluhu Hassan ataja miradi ya Bandari

‎Doreen Aloyce,Dodoma

‎Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa  amesema Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuimarisha sekta ya uchukuzi kama nguzo muhimu ya muunganiko wa kikanda na kimataifa, baada ya kufanikisha miradi mikubwa ya reli, bandari, usafiri majini na anga ndani ya siku 100 za Kipindi cha Pili cha uongozi wake.


Profesa Makame ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari Februari Mosi jijini Dodoma wakati akieleza Ahadi za Rais Samia kwa siku 100 tangu kuapishwa kwake ambapo  amesema Serikali imekamilisha taratibu za ufufuaji wa Reli ya TAZARA kufuatia kusainiwa kwa mkataba wa uboreshaji kati ya Tanzania, Zambia na Kampuni ya CCECC ya China. 

Mradi huo unatarajiwa kuanza kutekelezwa Juni 2026 na unalenga kuimarisha ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam, kukuza biashara ya kikanda na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha usafirishaji kwa nchi zisizo na bandari.

‎Prof. Mbarawa amesema huduma za reli ya SGR na MGR zimeendelea kuimarika, ambapo zaidi ya abiria 838,000 na tani zaidi ya 85,000 za mizigo zimesafirishwa, hali inayochochea biashara ya ndani na ya mipakani. Aidha, Serikali imepokea vichwa viwili vya treni na mabehewa 50 ya mizigo ili kuongeza uwezo na ufanisi wa reli

pia Serikali kupitia Wizara ya Uchukuzi imeweka kipaumbele kikubwa katika kulinda maisha ya wananchi na mali zao kwa kuimarisha mifumo ya utafutaji na uokoaji majini ili kuhakikisha hakuna mwananchi anayepoteza maisha wakati akijitafutia riziki ndani ya maji na hata pale ajali zinapotokea kunakuwepo na uwezo wa haraka wa kumuokoa mhusika. 

Waziri huyo amesema hatua zinazochukuliwa ni sehemu ya ahadi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan za kuboresha usalama wa usafiri, huduma za afya na ustawi wa wananchi hususan wanaoishi visiwani na maeneo ya mwambao. 

Ameeleza kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha ahadi hizo zinatekelezwa kwa vitendo kwa kuwekeza katika miundombinu, vifaa vya kisasa na rasilimali watu.

"Katika kipindi cha siku 100 zilizopita, Serikali imekamilisha ujenzi wa Kituo cha Kuratibu Utafutaji na Uokoaji cha Kikanda katika Ziwa Victoria mkoani Mwanza ambacho kitaimarisha usalama wa usafiri wa majini kwa kutumia mifumo ya kisasa ya mawasiliano, TEHAMA na vifaa vya uokoaji hali itakayoongeza ufanisi wa uokoaji pale majanga yanapotokea, " Amesema

No comments:

Adbox