Doreen Aloyce Dodoma
Watumishi wa Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa(Takukuru) , taasisi simamizi za maadili pamoja na mamlaka simamizi za maadili ya kitaaluma wametakiwa kuendelea kushirikiana na kuwekeza kwenye mikakati ambayo itaakisi na kuimarisha utendaji kazi wa wataalamu wanaotoa huduma kwa wananchi.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Crispin Chalamila,
wakati alipokuwa akifungua kikao kazi cha siku mbili cha kubadilishana uzoefu kuhusu masuala ya maadili na utawala bora baina ya taasisi simamizi za maadili ya utendaji na mamlaka simazi za maadili ya kitaaluma.
Chalamila amesema kuwa uwepo wa mawasiliano baina yao utasaidia kuimarisha hali ya uadilifu katika maeneo yao na kuchukua hatua kwa wale wachache watakaoonekana kwenda kinyume na utaratibu uliowekwa.
“Ninatoa rai kwetu wote kwamba, mawasilisho na majadiliano yetu yatuongoze kwenye ubunifu wa mikakati ya kuboresha misingi ya maadili ya utendaji na maadili ya kitaaluma kama njia mojawapo ya kuimarisha utoaji wa huduma katika utumishi wa umma, kudhibiti vitendo vya rushwa kwa lengo la kuleta ustawi kwa wananchi,”
alisema Chalamila
Hata hivyo, aliwasihi washiriki wa kikao hicho kuendeleza mawasiliano na ushirikiano kati yao taasisi simamizi za maadili pamoja na mamlaka simamizi za maadili ya kitaaluma ili kuimarisha hali ya uadilifu katika maeneo yao na kuchukua hatua kwa wale wachache watakaoonekana kwenda kinyume na utaratibu uliowekwa.
Mkurugenzi wa Usimamizi wa Maadili Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Felister Shuli, alisema kwa mujibu wa utafiti uliofanya mwaka 2021 na ofisi hiyo ulibaini kuwa suala la maadili nchini linaendelea kuimarika.
“Utafiti ule ulionyesha kuwa suala la maadili nchini linaendelea kuimarika kwani wananchi wengi hivi sasa wanaripoti matukio ya ufunjifu wa maadili lakini pia watumishi wa umma hivi sasa wanazingatia suala la maadili ya utumishi wa umma kazini,”alisema
Alisema licha ya mafanikio hayo bado zipo changamoto chache ikiwamo kwenye ngazi ya familia hivyo ipo haja ya kuendelea kukumbushana ili kuboresha utoaji huduma kwa wananchi.
Baadhi ya taasisi zilizoshiriki kwenye kikao hicho ni pamoja na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU),Ofisi ya Mkaguzi Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG),Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora,Mamlaka ya Udhibiti Manunuzi ya Umma (PPRA), Bodi ya Mkandarasi (CRB),Bodi ya Baraza la Wakunga na Wauguzi (TNMC).
Mwisho
No comments:
Post a Comment