Zikiwa zimesalia siku nne pekee kabla ya Watanzania kujitokeza kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani, baadhi ya viongozi wa dini kutoka Mikoa ya Singida na Dodoma wamewataka vijana kuepuka vishawishi vyovyote vinavyoweza kusababisha uvunjifu wa amani, wakisisitiza kwamba utulivu wa Taifa ni msingi wa maendeleo na umoja wa kitaifa.
Wakizungumza leo jijini Dodoma katika kongamano la viongozi wa dini mbalimbali kutoka Kanda ya Kati, viongozi hao wamehimiza vijana na wananchi kwa ujumla kuendelea kutimiza majukumu yao ya kijamii na kidini, huku wakielimisha jamii kuhusu umuhimu wa kulinda amani kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi.
Akitoa wito huo, Askofu Evance Chande wa Kanisa la Carmel Assemblies of God alisema vijana ndio nguvu kazi ya Taifa, hivyo wanapaswa kutumia nafasi yao kujenga badala ya kubomoa.
“Tunapaswa kuikumbatia amani kama tunavyokumbatia imani zetu. Uchaguzi ukipita, Tanzania inabaki kuwa moja, hivyo tusikubali kugawanywa kwa misingi ya kisiasa,” alisema Askofu Chande.
Kwa upande wake, Sheikh Mustapha Rajab, Sheikh wa Mkoa wa Dodoma ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maridhiano Kanda ya Kati na mgeni rasmi wa kongamano hilo, aliwahimiza wananchi kutii mamlaka na kufuata taratibu zinazotolewa na Serikali pamoja na viongozi wa dini.
“Amani si jambo la bahati mbaya, ni matokeo ya utii na hekima. Tukitii viongozi wetu na kuheshimu sheria, Taifa litaendelea kubaki salama,” alisema Sheikh Rajab.
Kongamano hilo lililolenga kuliombea Taifa amani na utulivu kuelekea uchaguzi, lilibebwa na kaulimbiu isemayo “Kupiga kura ni haki ya kila Mtanzania, amani na utulivu ni jukumu letu.
Viongozi hao walikubaliana kuwa jukumu la kulinda amani si la Serikali pekee, bali ni la kila mwananchi, na wakasisitiza umuhimu wa maombi, maelewano, na uvumilivu wakati wote wa mchakato wa uchaguzi.



No comments:
Post a Comment