Adbox

Saturday, 25 October 2025

MULIRO AONYA WANAOPANGA KUANDAMANA NA KUFANYA VURUGU DSM


Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amewaonya wale wote wanaopanga, kuratibu ama kutaka kushiriki kwenye uvunjifu wa amani ikiwemo kufanya vurugu na maandamano Oktoba 29, 2025, akisema Jeshi hilo limekula kiapo kulinda nchi pamoja na raia na mali zao.

Kamanda Muliro ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Oktoba 24, 2025 wakati wa kongamano la Vyuo na Vyuo Vikuu kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, Kongamano lililofanyika kwenye Ukumbi wa Ubungo Plaza na kuwashirikisha wanafunzi wa shule za Sekondari, Vyuo na Vyuo Vikuu, akiwataka Vijana pia kuwa waangalifu na kutafakari kuhusu misukumo na mihemko yao kulingana na aina na makundi ama watu wanaoambatana nao.

"Tukiwa kama watu tuliokula kiapo tunawaleza kuwa tutatimiza jukumu letu la kuhakikisha kuwa watu wanakuwa salama, watu wajitokeze kwa wingi kupiga kura, wafuate sheria na sisi tutakuwepo barabara kuwalinda wote wanaoenda kutimiza jukumu lao la Kikatiba la kwenda kupigakura. Siku hiyo kutakuwa hakuna maandamano wala hakuna vurugu, siku hiyo ni ya upigaji wa kura bila hofu."Amesema.

Kama Muliro pia amesisitiza kuwa Vijana kuwa na fikra chanya ama hasi katika kujadili jambo fulani sio kitu kibaya ila kuipeleka mitazamo hasi kwenye vitendo vya vurugu ndiyo kosa kisheria, akiwataka pia Vijana kulinda hatma zao kwa kuhakikisha nchi inakuwa na amani ili kuwawezesha kutimiza malengo na ndoto zao kiuchumi, kisiasa na Kijamii.

No comments:

Adbox