Adbox

Tuesday, 9 December 2025

Serikali yaweka kipaumbele katika kuhuisha majengo na kupanga upya miji mikubwa


Serikali imeweka kipaumbele katika kuhuisha majengo na kupanga upya miji mikubwa, hatua inayolenga kuongeza thamani ya makazi, kuboresha matumizi ya ardhi na kuvutia uwekezaji katika kipindi cha pili cha miaka mitano ya Serikali ya Awamu ya Sita.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo amesema mpango huo utahusisha ubia kati ya wananchi na sekta binafsi ili kubomoa nyumba chakavu, kujenga majengo mapya ya ghorofa na kuwapa wakazi sehemu za makazi na biashara ndani ya miradi hiyo.

Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam siku ya Jumatatu, Prof. Mkumbo amesema Serikali tayari imeainisha maeneo matatu ya kuanzia Vingunguti, Buguruni na Manzese kwa mkoa wa Dar es Salaam ambapo michakato ya kuwavutia wawekezaji itatangazwa rasmi, huku wakazi waliopo wakihakikishiwa kunufaika moja kwa moja kupitia mfumo wa kupata ‘floor’ zao za makazi na biashara katika majengo mapya.

Waziri huyo amesema mageuzi ya miji ni sehemu ya mkakati mpana wa kufungua fursa za uchumi, kuongeza ajira na kuboresha ubora wa maisha katika maeneo ya mijini. Ameeleza kuwa matumaini ya Serikali ni kuona miji ya Dar es Salaam na baadaye mingine nchini ikiwa na makazi yaliyopangwa vizuri na miundombinu ya kisasa.

Amesema sambamba na kuhuisha miji, Serikali inaelekeza nguvu katika kufungua maeneo mapya ya utalii tofauti na yale yanayofahamika sana kama Ukanda wa Kaskazini, huku akitaja Hifadhi ya Taifa ya Ruaha kama moja ya maeneo makubwa yenye uzuri wa kipekee lakini ambayo hayajafunguliwa kikamilifu. Pia ameeleza kuwa utalii wa fukwe haujatumiwa ipasavyo licha ya Tanzania kuwa na mwambao mrefu uliojaa vivutio.

Prof. Mkumbo amesema Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi ya ndani na nje ya nchi ili kuongeza uwekezaji katika utalii, ujenzi na miundombinu, hatua anayosema itachochea ukuaji wa mapato ya taifa na kupanua ajira kwa vijana.

No comments:

Adbox