Adbox

Tuesday, 9 December 2025

JESHI LA POLISI LAKANUSHA TAARIFA ZA UPOTOSHAJI MTANDAONI, LATHIBITISHA USALAMA NCHINI KUWA SHWARI



Na Mwandishi wetu, Dodoma

Jeshi la Polisi nchini limekanusha taarifa zinazoenezwa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu kuwepo kwa maandamano leo Desemba 9, 2025, na kusisitiza kuwa hadi majira ya mchana hali ya usalama nchini kote ni shwari.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi, Makao Makuu ya Polisi Dodoma,David Misime vyombo vya ulinzi na usalama vinaendelea kuimarisha ulinzi na kulinda maisha ya wananchi pamoja na mali zao kama ilivyo jukumu lao la msingi.

Polisi imeeleza kuwa picha na video zinazosambazwa mitandaoni zikidaiwa kuonyesha maandamano yanayoendelea leo si sahihi, bali ni matukio ya zamani na kwamba baadhi ya picha hizo zinatoka katika matukio ya Oktoba 29, 30 na 31 mwaka 2025, huku zingine zikitoka miaka ya nyuma ikiwemo tukio la Juni mwaka huu ambalo lilihusisha sherehe za jando za jamii ya Wamaasai zilizofanyika katika msitu wa TANAPA jijini Arusha.

Jeshi hilo limekumbusha kuwa maandamano yaliyokuwa yanatajwa kama “maandamano ya amani” yalipigwa marufuku tangu Desemba 5, 2025, baada ya kubainika hayakukidhi matakwa ya kisheria ikiwemo Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na Sheria ya Polisi na Polisi Wasaidizi, Sura ya 322.

Aidha, Polisi imetoa wito kwa wananchi kuendelea kufuata sheria za nchi na kupuuza taarifa za upotoshaji, kwa manufaa ya amani na usalama wa Taifa.

No comments:

Adbox