Na Doreen Aloyce,Dodoma
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Asha-Rose Migiro, ametaka kuanzishwa kwa mazungumzo ya kitaifa ya maridhiano huku akiwasisitiza wanawake nchini kuchukua jukumu la uongozi katika kulinda na kuimarisha amani. Wito huo umetolewa wakati wa ufunguzi wa Jukwaa la Wanawake 2025 lililofanyika jijini Dodoma chini ya kaulimbiu “Mama ni Amani”.
Katika hafla hiyo, washiriki walioneshwa makala ya video iliyodokeza matukio ya vurugu za Oktoba 29, 2025, ikionesha kiwango cha uharibifu wa mali na taarifa za vifo, ingawa idadi kamili ya waliofariki haikutajwa. Dk. Migiro alisema matukio hayo hayalingani na utamaduni wa Tanzania wa mshikamano na utulivu, hivyo kuhitaji hatua za makusudi kurejesha hadhi ya taifa.
Amefafanua kuwa zaidi ya asilimia 50 ya Watanzania ni vijana na ndiyo maana wanawake wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika malezi, uongozi wa majadiliano ya maridhiano na kuzuia kurudiwa kwa matukio ya vurugu.
Washiriki wa jukwaa hilo walitoa maoni mbalimbali kuhusu nafasi ya mwanamke katika kudumisha amani.
Kate Kamba alisisitiza kuwa wanawake ni walimu wa kwanza wa familia na wanabeba jukumu muhimu la kujenga misingi inayoweza kuzuia machafuko ya baadaye. Alionya kuwa bila kuwekeza katika malezi bora, taifa linaweza kupoteza mwelekeo wake.
Sifa Swai, kwa upande wake, alisema changamoto za usalama wa amani zimehamia zaidi kwenye mitandao ya kijamii ambako taarifa potofu husambaa kwa kasi, hivyo kuwaathiri hasa vijana. Aliongeza kuwa misukosuko katika biashara zinazomilikiwa na wanawake huathiri moja kwa moja ustawi wa familia na inaweza kuchochea migogoro ya kijamii.
Kwa pamoja, washiriki walikazia umuhimu wa sauti ya mwanamke katika kuponya makovu ya kijamii, kudumisha umoja na kuongoza juhudi za maridhiano nchini.


No comments:
Post a Comment