Na Doreen Aloyce, Dodoma
NAIBU Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Dennis Lazaro Londo, amewahakikishia waandishi wa habari nchini kuwa Serikali itaendelea kulinda uhuru wao wa kujieleza pamoja na kuhakikisha wanatimiza majukumu yao kwa usalama na weledi.
Mhe. Londo amezungumza hayo ljijini Dodoma katika mafunzo ya waandishi wa habari yaliyoandaliwa na Misa Tanzania yaliyowaleta pamoja Wanahabari 100 kutoka maeneo mbalimbali nchini, ambapo Londo amesema Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi itaendelea kushirikiana na wadau wa habari katika maeneo yote yanayohusu usalama kwa waandishi wa habari.
Aidha, amebainisha kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweka msukumo mkubwa katika kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi, sambamba na kulinda uhuru wa vyombo vya habari.
" Falsafa ya Mhe. Rais kupitia “4R” zinaipa tasnia ya habari nafasi muhimu katika kulinda amani, kuimarisha umoja wa kitaifa na kuendeleza mijadala yenye tija kwa jamii." Amesema Londo.
Edwin Soko ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika – Tawi la Tanzania (MISA Tanzania), ametahadharisha kuwa uandishi unaolenga kugawa jamii unadhoofisha misingi ya amani ambayo nchi imeijenga kwa miaka mingi,huku akisisitiza kuwa vyombo vya habari vinapaswa kujikita kuandika habari ambazo zitaleta umoja na mshikamo sio kuchochea mgawanyiko na uhasama kwa taifa.
“Hii ndiyo Tanzania, sisi ndiyo Watanzania,tukiruhusu nchi yetu ikawaka moto hatuna pa kwenda.Wapo wanaolaumu na kuona kama vyombo vya habari havijatimiza wajibu wake Oktoba 29,2025 wakati wa uchaguzi, na kusahau kuwa vyombo vya habari havilengi kwenye kuiboa jamii bali kuijenga ,”amesema Soko.
Pia Soko ametumia fursa hiyo,kusisitiza umuhimu wa waandishi na vyombo vya habari kuwa uhuru na kufanya kazi zao kwa kufuata maadili ya uandishi bila msukumo au shinikizo kutoka kwa watu binafsi.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha SAUT Mwanza, Dkt. Dotto Bulendu, akizungumza wakati akiwasilisha mada kuhusu umuhimu wa uandishi wa habari jengefu,amesema jamii inahitaji taarifa zenye mizania sahihi pia sauti za vijana zishirikishwe na zisikike katika mambo ya kitaifa.
“Nadhani uandishi huu utatusaidia kuondoka hapa tulipo,wananchi wanataka kuona serikali ikiwajibika na ikija na majibu pia wanahitaji kusikilizwa. Kwa maana hiyo waandishi tunatakiwa kuwa kiunganishi cha makundi yote na kuepuka habari zinazoibua taharuki,”amesema Bulendu
Kwa upande wake Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini,DCP David Misime,akiwasilisha mada ya wajibu wa vyombo vya habari katika kukuza amani amesema ni pamoja na kuandaa na kutangaza taarifa nyingi zenye maudhui ya kuhımıza na kuimarisha umoja, mshikamano, amanı,utulivu na upendo utakaowezesha maridhiano.
“Yaliyotokea Oktoba 29,2025 hakuna ambaye hakuonja machungu yake.Tumejifunza,binafsi nimejifunza namna ya umuhimu wa amani,”amesema Misime.
DCP.Misime amesema, waandishi wanapaswa kubuni na kukuza majadiliano yanayojenga badala ya kugawa wananchi na taifa,kuzingatia ukosoaji wa kihabari unaojenga na wenye lengo la kuboresha,kuripoti mapungufu bila kuchochea migogoro,kuchambua masuala kwa uadilifu pamoja na kutoa majibu mbadala
Amesema,waandishi wa habari ni watu muhimu na wana mchango mkubwa katika kukuza na kuimarisha usalama, utulivu na amani.
Mwisho.

