Na Doreen Aloyce, Dodoma
TAASISI ya Uhasibu Arusha (IAA) imeongeza kasi ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati inayolenga kuimarisha ubora wa elimu, kukuza uchumi wa kidijitali na kuboresha kwa kiwango kikubwa mazingira ya kufundishia na kujifunzia, kwa kuwekeza zaidi ya shilingi bilioni 42 katika ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya chuo katika kampasi zake mbalimbali nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma Februari 20,2026, Prof. Eliamani Sedoyeka, Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), amesema uwekezaji huo unahusisha utekelezaji wa Madarasa Janja Mahiri ya Akili Unde (AI Smart Classrooms), ujenzi wa Kituo cha Kisasa cha Data, utoaji wa Elimu Mseto, ongezeko la uwezo wa intaneti, muunganisho wa MPLS pamoja na ujenzi wa Kituo cha Umahiri cha TEHAMA.
Amesema hatua hiyo inalenga kuongeza ubunifu, ajira na ushindani wa taifa kimataifa.
"Mbali na uwekezaji wa teknolojia, IAA inaendelea na ujenzi wa majengo ya taaluma, hosteli na utawala katika kampasi za Arusha, Babati, Dodoma na Songea," Amesema
Na kuongeza " Zaidi ya shilingi bilioni 18 zimetumika kujenga hosteli katika kampasi za Arusha na Babati ili kuwahakikishia wanafunzi, hususan wa kike, malazi salama na rafiki, " Amesema Prof. Sedoyeka
Aidha amesema Kupitia Mradi wa HEET, taasisi hiyo pia inanufaika na ujenzi wa majengo ya taaluma katika kampasi za Babati na Songea yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 32 kwa pamoja, hatua inayotarajiwa kuongeza ubora wa mazingira ya kufundishia na kujifunzia.

